|

Mandela Kuondolewa Mashine za Kumsaidia Kupumua.


Johannesburg. Madaktari wanaomtibu Nelson Mandela wameishauri familia yake iondoe mashine zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’. Taarifa hizo zimo kwenye viapo vya wanafamilia hao ambavyo viliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Eastern Cape, Mthatha ambako familia hiyo ilikuwa ikipambana kurejesha mabaki ya miili ya watoto wa Mandela kutoka Mvezo kwenda Qunu. Wanafamilia 16 walifungua kesi mahakamani akiwemo mkewe Graca Simbine Machel Mandela na mtalaka wake Winnie Madikele Mandela dhidi ya walalamikiwa watatu akiwemo Zwelivelile Mandle Sizwe Dalibhenga, maarufu Mandla, ambaye ni mjukuu wa Mandela. Mandela ambaye aliongoza vita ya ubaguzi wa rangi enzi za utawala wa mabavu wa Makaburu, alilazwa tangu Juni 8 mwaka huu katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliyopo Pretoria ambako hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya sana. Juzi na jana afya ya kiongozi huyo ilizua utata na mvutano mkubwa kutokana na kutolewa kwa taarifa kwamba madaktari wanaomtibu walishauri familia yake iondoe mashine zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’.

 Hati za viapo hivyo zinathibitisha kwamba Mandela anapumua kwa mashine na madaktari wanaomtibu waliishauri familia kuondoa mashine hizo suala ambalo limebaki katika mikono ya familia. Viapo hivyo viliandikwa Juni 26 mwaka huu na kuwasilishwa mahakamani Juni 28, lakini havikuwahi kutolewa hadharani hadi Julai 3, wakati uamuzi wa kesi ulipotolewa na kumwamuru mjukuu wa Mandela, Mandla arejeshe mabaki ya miili ya watoto wa babu yake Qunu. Mabaki hayo yaliyohamishiwa Mvezo 2011 ni ya watoto wa Mandela ambao ni Madiba Thembekile aliyefariki kwa ajali ya gari 1969, Makgatho aliyefariki 2005 na binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) aliyefariki dunia 1948 akiwa mtoto mchanga.

 Mabaki hayo yalizikwa juzi Alhamisi katika makaburi ya familia, Qunu ikiwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama. Kati ya juzi na jana, Ikulu ya Pretoria ililazimika kutoa taarifa mbili; moja muda wa jioni na nyingine usiku wa kuamkia jana ikiwa ni hatua ya kuondoa hofu iliyokuwa imeanza kusambaa baada ya vyombo vya habari kuweka bayana kilichoandikwa katika viapo vya mahakama. Hoja kubwa ambayo imekuwa ikijadiliwa ni kwa jinsi gani viapo vya mahakama vionyeshe kwamba uwezekano wa Mandela kuendelea kuishi ni mdogo huku Serikali ikitoa taarifa kwamba hali ya Mandela ni imara licha ya kwamba yu mahututi. Katika taarifa zote mbili Rais Jacob Zuma kupitia kwa msemaji wake, Mac Maharaj aliweka wazi kwamba Mandela ‘siyo mtu wa kufa wakati wowote’ kama ilivyoripotiwa ikasisitiza kwamba hali yake imeendelea kuwa imara licha ya kwamba ni mgonjwa sana.

Source: Mwananchi.

Posted by Unknown on 3:28 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for "Mandela Kuondolewa Mashine za Kumsaidia Kupumua."

Leave a reply

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...