Askari Polisi Akikosea, Akashtakiwe wapi?
Picha Kwa Hisani ya Kipanya |
Kimaadili, kazi ya msingi ya askari polisi ni kulinda raia na mali zao, wajibu wa msingi ambao umedumu kwa miaka mingi.
Hata hivyo, dhana ya polisi nchini kuwa walinzi wa raia na mali zao imeanza kukosa uhalisia na huenda huko tuendako ikapotea na askari haoi kuchukuliwa kama adui wa raia na mali zao.
Ninasema hivi kutokana na matukio ya uonevu wa wazi unaofanywa na askari hao dhidi ya raia wasio na hatia. Ipo mifano mingi ya unyanyasaji wa polisi dhidi ya raia.
Hapa ninazungumzia askari wa usalama barabarani, askari wa doria, askari wa upelelezi au hata askari wa vyeo vya juu ambao wengi wao hutumia nguvu nyingi na wakati mwingine silaha kupambana na mwananchi wasio na silaha.
Yaani, kila mmoja kwa nafasi yake anapuuza kwa makusudi wajibu wake kuwalinda raia na mali zao, badala yake anaamua kutumia mabavu ili kujinufaisha huku akimdidimiza mwananchi. Ipo mifano ya wazi. Ni matukio ya matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi yanayofanywa na askari wetu katika sehemu mbalimbali za nchi.
Mfano hai ambao hautafutika mioyoni mwa wananchi ni mauaji ya kikatili yaliyofanywa hadharani na askari polisi dhidi ya mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten, Daudi Mwangosi ambaye aliuawa hadharani na askari polisi kule Nyololo, Mufindi mkoani Iringa mwaka jana kwa kutupiwa bomu la kutoa machozi.
Mbali na mauaji ya Mwangosi, yapo matumizi ya nguvu na mauaji kadhaa kwa raia yanayofanywa na polisi dhidi ya raia ambayo yanamweka askari mbali na mwananchi na kuifuta ile dhana iliyozoeleka kuwa Jeshi la Polisi ni walinzi wa raia na mali zao.
Mbali na hayo matukio yanayolalamikiwa kila kukicha na wananchi pamoja na watetezi wa haki za binadamu, upo unyanyasaji mkubwa unaofanywa na askari polisi dhidi ya raia mmoja mmoja ambao usipopigiwa kelele au kukemewa au kuingilia kati na Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Said Mwema huenda kukajengeka uadui mkubwa kati ya raia na askari polisi nchini kote.
Mbali na matukio hayo makubwa, yapo matukio mbalimbali ya unyanyasaji yanayofanywa na askari polisi katika vituo vya polisi ambapo huwapiga watuhumiwa, kuwapora fedha zao pale wanapofika kama watuhumiwa wa uhalifu katika vituo vidogo.
Askari polisi wa vituo vidogo nchini wanawatambia raia na watuhumiwa kuwa mtu yeyote anapokuwa chini ya polisi hana haki yoyote na anaweza kupigwa hata kuuawa na hakuna sheria yoyote inayoweza kuchukuliwa dhidi ya muuaji kwa kuwa eti, yeye askari yupo kazini.
Kitendo cha polisi kupiga na kuua, iwe kwa raia asiye na tuhuma au mtuhumiwa si moja ya kazi ya askari. Mabango mengi yaliyoandikwa na kubandikwa katika vituo vya polisi yakielekeza mambo mbalimbali yamebakia kama ya biashara barabarani na hakuna ukweli wowote wa kile kinachoandikwa maana yameandikwa nao wenyewe.
Askari wanatafsiri kinyume maneno ‘police force’ kuwa yana maana ya askari kutumia nguvu na kwamba wanapoua mtuhumiwa au raia yeyote iwe kituoni au mahali pengine popote, hakuna utaratibu ulio wazi wa kuwachukulia hatua eti kwa kuwa hiyo ni moja ya kazi ya askari polisi anapovaa magwanda ya jeshi hilo.
Jukumu muhimu na la msingi walilo nalo askari kwa jeshi lao ni kutambua kuwa wapo kwa ajili ya ulinzi wa raia na mali zao, basi! Na raia anapokumbana na uonevu badala ya kupambana au kutumia nguvu kupata haki yake anapaswa kukimbilia polisi kutafuta msaada wa ulinzi na usalama wake na mali zake na si vinginevyo.
joycemmasi@yahoo.co.uk 0784253436
Imetoka: HAPA
Posted by Unknown
on 11:34 PM. Filed under
Habari za Kitaifa,
Udaku wa Tanzania
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0.
Feel free to leave a response