TRL Waingiza Hasara ya zaidi ya 1.2M Kila Siku
Habari Katika Gazeti la Mwananchi
Dar es Salaam. Licha ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kudai kupata hasara ya wastani wa Sh1.2 milioni kwa siku kutokana na uendeshaji wa treni ya Dar es Salaam, imeshidwa kuelezea bayana hasara hiyo ikidai Wizara ya Uchukuzi inajua yote.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa TRL, Kipalo Kisamfu, alikaririwa akidai wamekuwa wakiendesha mradi wa usafirishaji abiria kwa hasara kiasi cha kufikiria kufungwa kwa mpango huo.
Gazeti hili lilitaka kufahamu mchanganuo halisi wa hasara na gharama za uendeshaji kwa siku, ikiwamo gharama za mafuta na posho kwa wafanyakazi, lakini mkurugenzi huyo alishindwa kuonyesha.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez, alisema suala la hasara halina umuhimu kuliongelea sasa, kwa sababu faida zinazotokana na usafiri huo kwa wananchi ni kubwa.
“Treni hii ilianzishwa maalumu kusaidia wakazi wa Dar es Salaam kuondokana na tatizo la usafiri hasa nyakati za asubuhi na jioni,” alisema Maez na kuongeza:
“Hivyo suala la hasara halina msingi sana kwani haikuanzishwa kwa kuangalia faida zaidi, hata nauli tunayotoza ya Sh400 inadhihirisha hilo.”
Alisema huduma ya usafiri inasaidia wananchi kuwahi sehemu za kazi na kwamba, kwa siku wanasafirisha wastani wa abiria 5,000.
Ofisa Masoko Mfawidhi wa TRL Hassan Shaaban, aliwahi kukaririwa kuwa ukosefu wa sehemu ya kugeuzia na matumizi ya vichwa na mabehewa, ambayo siyo maalumu kwa usafiri wa mjini ni mojawapo wa sababu zinazochangia hasara ya uendeshaji kwa treni ya Dar es Salaam.
Posted by Unknown
on 2:13 AM. Filed under
Habari za Kitaifa
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0.
Feel free to leave a response