"Afisa wa JWTZ Aliyetoroka si Mnyarwanda" Meja Komba
Dar es Salaam. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linamtafuta ofisa wa jeshi hilo, Luteni Kanali, Colestine Seromba, baada ya kutoroka na kuelekea kusikojulikana.
Ofisa huyo aliyekuwa Mkufunzi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Kompyuta kilichopo Dar es Salaam, anasadikiwa kutoroka na nyaraka muhimu za jeshi hilo tangu Desemba 18, mwaka jana.
Msemaji wa jeshi hilo, Meja Erick Komba akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi jijini humo jana alisema, Seromba alikuwa na tuhuma za makosa ya kijeshi na ndiyo sababu ya kutoroka kwake.
“Wakati mchakato wa kumfungulia mashtaka ukiwa unaendelea ofisa huyo alitoroka usiku wa Desemba 17 kuamkia 18 mwaka jana, hivyo ofisa huyu ni mtoro kwa kipindi cha ziadi ya miezi minane,” alisema Meja Komba na kuongeza:
“Kijeshi kosa la utoro halifutiki, yaani halina ‘Time Bar’. Kwa maana hiyo bado ofisa huyu anaendelea kutafutwa na akipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.”Meja Komba alisema ofisa huyo ni Mtanzania mzaliwa wa Kijiji cha Rukira mkoani Kagera na si Mnywaranda kama ambavyo baadhi ya taarifa zinavyoenezwa.
Akijibu swali aliloulizwa kuhusu ofisa huyo kuwa Mkuu wa Chuo hicho, Meja Komba alisema alikuwa mkufunzi wa masomo ya kompyuta na taarifa nyingi alizokuwa nazo ni zile zilizowahusu wanafunzi yaani mahudhurio na matokeo yaliyowahusu wanafunzi.
“Mkuu wa chuo hicho hakuwa yeye alikuwa Kanali Obeid ambaye naye amestaafu miezi sita sasa, lakini jeshi lilipoanza uchunguzi dhidi yake alikabidhi vitendea kazi vyake vyote,” alisema Meja Komba.
Chanzo: Mwananchi
Posted by Unknown
on 1:46 AM. Filed under
Habari za Kitaifa
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0.
Feel free to leave a response