|

Wawili Mbaroni kutokana na Mauaji ya Bilionea wa Madini Arusha

Marehemu Msuya Enzi za Uhai Wake

Arusha. Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao mtaa wa Kairo, Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha, kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’ zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,” alidokeza polisi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea zaidi baada ya simu yake kutokupatikana.
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema hata hiyo jana, timu ya wapelelezi kutoka Moshi wakiongozwa na RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi walikuwapo jijini hapa na watuhumiwa hao.
Uchunguzi zaidi wa polisi kuhusu mmiliki halali wa pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na vijana wawili waliotekeleza mauaji hayo, zimebaini kuwa bado inamilikiwa na kampuni moja ya Dar es Salaam iliyouza pikipiki hiyo.
Habari zaidi zinadai kuwa pikipiki hiyo ilinunuliwa mahususi kwa ajili hiyo na mwanamke mmoja ambaye hafahamiki na ilinunuliwa katika duka ambalo ni tawi la kampuni iliyoingiza pikipiki hiyo lililopo Arusha.
Mfanyabiashara huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho, huko Mirerani, aliuawa baada ya kuitwa kwa simu na wauaji waliojifanya ni vijana wenye madini ya Tanzanite waliotaka kumuuzia marehemu.
Source: Mwananchi

Posted by Unknown on 3:07 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for "Wawili Mbaroni kutokana na Mauaji ya Bilionea wa Madini Arusha"

Leave a reply

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...