Luteni Mutabuzi aliyekuwa mlinzi wa Rais Paul Kagame |
Umoja wa mataifa jumatano wiki hii ilitoa pingamizi kali kwa serikali ya Uganda kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya utekaji na majaribio ya mauaji ya wapinzani wa Rais Rwanda bwana Paul Kagame wanaoomba ukimbizi nchini humo.
Hayo yamekuja masaa kadhaa baada ya kugundulika kuwa walinzi wawili wa zamani wa Rais Paul Kagame waliokuwa wamepewa ukimbizi nchini Uganda, mmoja hajulikani alipo na mwingine alipatikana akiwa anasafirishwa kupelekwa nchini Rwanda kwa kibali cha bandia cha shirika la kimataifa la polisi dunia - Intelpol.
Bwana Innocent Karisa hajulikani alipo na Luteni Joel Mutabazi ambaye alitekwa na polisi wa Uganda kwa sababu zisizojulikana alipatikana akisafirishwa kuelekea nchini Rwanda kwa kutumia kile ambacho baadae kilijukana kama kibali bandia cha jeshi la polisi la kimataifa- Intepol.
Luteni Mutabazi, alikuwa mlinzi wa Rais Kagame kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa, kuteswa, kufungwa na kutaka kuuwawa na Raisi kagame kabla hajapata mpenyo wa kukimbilia nchini Uganda.
Siku za karibuni Luteni Mutabazi, alinukuliwa hadharani akisema kwamba rais Kagame ni dikteta na muuaji na kwamba yuko tayali kuyaweka hadharani mambo yake yote ya gizani anayofanya rais huyo aliyekuwa kipenzi cha nchi za magharibi.
Katika maelezo yake, Luteni Mutabazi alidai kuwa rais Kagame pia alihusika na mauaji ya maelfu ya wakimbizi wa kihutu miaka miwili baada ya mauaji ya halaiki, yeye akiwa mlinzi wake alikwenda naye katika gereza moja lililoko nje kidogo ya mji wa Kigali ambako alikwenda kushuhudia miili ya maiti za wahutu ambayo ilikuwa imewekwa kwenye lori kubwa.
Luteni Mutabazi alidai, mwaka huo huo 1996, Kagame akiwa pia waziri wa ulinzi walienda mara mbili kukagua miili ya wakimbizi wa kihutu katika gereza hilo la siri ambalo linasimamiwa na idara ya usalama ya jeshi la Rwanda. Kwa hiyo kutekwa kwake kunahusishwa na kauli yake hiyo.
Kwa muda mrefu Rais Kagame amekuwa akituhumiwa kuhusika na mauaji ya wapinzani wake ambao wengi walikuwa washiriki wake, na pia amekuwa akituhumiwa kutumia mashtaka ya mauaji ya halaiki kuwabambikizia kesi wapinzani wake ambao anawaona kuwa tishio. Hata hivyo Kagame amekuwa akikanusha.
Matukio hayo mawili ya utekaji yamechochea kuchukuliwa hatua za haraka na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, shirika hilo jana lilijitokeza kuihoji serikali ya Rais Yoweri Museveni ambayo licha ya kuwapokea wapinzani wa Kagame lakini pia bado ni mshiriki wake mkubwa, limeitaka serikali ya Uganda kulinda na kufuata kwa dhati sheria za kimataifa za kuhakikisha usalama kwa wakimbizi na waombaji wa ukimbizi.
Msemaji wa UNHCR, Kitty Mckinsey amesema shirika lake limetuma waraka wenye msisitizo mkubwa katika serikali ya Uganda, kufuatia matukio ya hivi karibuni ya utekaji wa wakimbizi na waombaji wa ukimbizi pamoja na majaribio ya mauaji ya Joel Mutabazi, yaliyofanywa na watu wanaoonekana kuwa siyo raia wa Uganda.
Idadi ya maafisa wa zamani wa serikali ya Kigali katika siku zilizopita wamekuwa wakiitumia Uganda kwenda uhamishoni au kubaki nchini humo, hali iliyosababisha kudhoofisha mahusiano ya serikali za Kampala na Kigali.
Kwa mujibu wa gazeti moja la nchini Uganda ambalo liliongea na maofisa wa juu wa serikali ya Uganda wameripoti kuwa hati ya Interpol iliyotumika kumkamata Mutabazi ilikuwa ya bandia, lakini maofisa hao hawakutaka kutaja majina yao kwa kuhofia kuhatarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
Luteni Mutabazi anaripotiwa kulala kituo cha polisi cha Jinja road baada ya kuokolewa dakika za mwisho, alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Namugongo nje ya mji siku ya Jumanne usiku kwa nguvu, na watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi la polisi waliofanya kosa la kumkamata na kujaribu kumpeleka Rwanda.
waziri wa wizara ya maandalizi ya majanga na wakimbizi bwana Musa Ecweru anayeshughulikia kesi ya bwana Mutabazi jana alisema polisi wao walifanya makosa ya kumkamata na kujaribu kumhamishia Rwanda.
Alipoulizwa kwa nini polisi walitumia kibali bandia cha Intepol kumkamata, afisa wa jeshi hilo la kimataifa Asan Kasingye alisema hawezi kusema lolote juu ya hilo.
Mwaka 2012 watu wasiojulikana waliokuwa na silaha walijaribu kumuuwa luteni Mutabazi katika nyumba yake ya zamani huko Kasangati.
Wakati huo huo, Innocent Karisa mlinzi wa zamani wa Kagame, hajulikani alipo tangu jumatano hivyo kuhamasisha msako mkali unaofanywa na wajumbe wa familia yake. Bwana Karisa alitoweka kutoka Kigali na kutafuta ukimbizi nchini Uganda mwaka 2012.
Source: swahilitv.