Mwakyambe Kuwataja "Wauza Unga Leo"
style="font-size: 14.545454025268555px; line-height: 1.4em; margin: 0px; padding: 0px;">Dar es Salaam. Siku moja baada ya kufanya ziara ya ghafla Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema leo ataweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini.
Dk Mwakyembe juzi alifanya ziara hiyo JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kashfa ya kupitishwa kwa dawa za kulevya na baadhi ya Watanzania wakiwamo wasanii kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, hatua ya waziri huyo imekuja siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili kuanzia juzi, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya Jitambue Foundation, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, Dk Mwakyembe alisema yuko tayari kufa katika vita hivyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake jana, Dk Mwakyembe alisema: “Kesho (leo) nitawataja wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kwa sasa nakamilisha ushahidi wa kutosha ikiwa ni pamoja na picha za wahusika.”
Aliwaonyesha waandishi wa habari picha ya mtuhumiwa mmoja ambaye alisema alikamatwa saa nane baada ya waziri huyo kufanya ziara uwanjani hapo. “Ninataka watu wafahamu wanaoliingiza taifa hili katika aibu hii, ambayo inasababisha Watanzania wasiaminike katika viwanja vya ndege vya mataifa mengine.”
“Hatuwezi kuwa taifa la kuogopaogopa, hii ni vita ya kusafisha nchi yetu, kwani ni nani mwenye mkataba na Mungu kuwa ataishi milele?” alihoji Waziri huyo alipokuwa akijibu swali kuwa suala la kuwataja watu wanaowafichua wasafirisha unga linaweza likaweka rehani maisha yake.
“Kama hupendi joto usiingie jikoni”, alisema.
Akizungumzia watendaji wa JNIA kuhusiana na dawa za kulevya, alisema: “Mfanyakazi yeyote atakayebainika kuhusika kuwasaidia wasafirisha unga atafukuzwa kazi na ambaye atafanya juhudi ya kuwakamata wasafirishaji hao atapewa zawadi.”
“Kuna watu wanadhani tunafanya mzaha katika jambo hili. Jana baada ya mimi kuondoka usiku wa saa 2:30 huyu (kijana aliyekamatwa) akaingia na mzigo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa alikamatwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Aliiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwatunuku wafanyakazi waliofanikisha kukamatwa kwa kijana huyo.
Akizungumzia hali ya Uwanja wa JNIA baada ya kufanya ziara juzi, Dk Mwakyembe alisema tatizo halipo kwenye vitendea kazi, bali wafanyakazi wasiokuwa waaminifu.
Habari kwa Hisani ya Gazeti la : Mwananchi
Posted by Unknown
on 7:04 AM. Filed under
Habari za Kitaifa
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0.
Feel free to leave a response