|

Tanzania na Biashara ya Viungo vya Maiti.



Habari kwa Hisani ya Global Publishers

Na Waandishi Wetu
OPARESHENI Fichua Maovu ‘OFM’ ya Global Publishers bado iko mitaani ikiibua mambo, wiki hii ilitia timu Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani kilomita chache kutoka jijini Dar es Salaam.
Kiganja cha binadamu.
Safari hiyo ilifanywa baada ya kupokea ‘mashitaka’ kwamba, wafanyakazi wa mochwari moja katika hospitali kubwa mjini Kibaha wamekuwa wakiuza viungo vya binadamu.
VIUNGO VINAVYOUZWA
Kwa mujibu wa chanzo, viungo vinavyouzwa katika mochwari hiyo ni sehemu za siri za jinsi zote, viganja, ndimi na miguu.
WALIOKUFA KWA AJALI DILI ZAIDI
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, viungo vya maiti za watu waliokufa kwa ajali vina dili zaidi kwa sababu havijadhoofika kama wale waliokufa kwa kuugua.
“Tena nawaambia OFM, viungo vya watu waliokufa kwa ajali ni mali sana, wanasema viungo vyao ni imara kuliko wale waliokufa kwa kuugua,” kilisema chanzo.
Mochwari.
VINAPATIKANAJE, WATEJA WAO AKINA NANI?
Sosi akaendelea kuweka wazi kwamba, watu wanaofanya kazi mochwari huvikata viungo hivyo wakati wa kuosha miili ya marehemu na kuhifadhi kwa ajili ya wateja wao ambapo wengi ni waganga wa kienyeji.
DILI LINGINE
Mbali na ‘bidhaa’ hizo, maji yaliyooshewa maiti na sanda navyo vilitajwa kuwa ni dili kubwa kwa wafanyakazi wa mochwari.
“Halafu yale maji yanayooshewa maiti na sanda au shuka ambalo hutumika kufunikwa maiti pia ni dili kubwa sana, waganga wanachukua kwa ajili ya kwenda kufunikia kesi mbaya za watu,” alisema mtoa habari wetu.
Wanahabari wa GPL wakiwa mzigoni.
MAITI ZA WAKRISTO ‘ZINAONEWA’ ZAIDI
Mtoa habari akasema maiti za Wakristo ndiyo huongoza kwa kufanyiwa mchezo huo kwa vile ndugu zao huwapa kazi ya kuosha wafanyakazi na wao kusubiri nje.
Akasema kwa Waislamu ni ngumu kidogo kwani wao wakati wa maiti wao kuoshwa ndugu wawili watatu huingia kusaidia ili kwenda sawa na kanuni za uoshaji wa imani hiyo.
Mtoa habari huyo alizidi kudai kwamba, maiti nyingi za Wakristo huagwa na ndugu kwenda kaburini zikiwa na upungufu wa viungo ila kwa sababu hakuna utamaduni wa kukagua hakuna anayejua. Inatisha sana!

OFM WAINGIA MZIGONI
Baada ya kupata taarifa hizo, hivi karibuni mapaparazi wetu makini walitia timu kwenye hospitali hiyo ambayo hupokea maiti nyingi za watu waliopata ajali katika Barabara ya Morogoro Dar es Salaam.
Walipata bahati ya kupokelewa na mfanyakazi wa mochwari ambapo baada ya salamu walijitambulisha kwa majina ya bandia, Paschal na Fanuel.
Walisema  wao ni wafanyabiashara wa samaki tokea Mwanza na wanataka viungo vya wanadamu vilivyopo mochwari hapo.
Mfanyakazi huyo aliweka bayana kwamba, kuna mikono na sehemu za siri za kiume, kama wako tayari wanaweza kuuziwa. Bei ni shilingi milioni moja (1,000,000) mpaka laki mbili (200,000) kutegemea na ukubwa wa kiungo chenyewe.
Ili kudhihirisha hilo, mfanyakazi huyo alikwenda kutoa ‘sampo’ ya viungo hivyo na kuambiwa kama wapo tayari watoe mkwanja biashara ifanyike mara moja.
IGP Said Mwema.
MAPAPARAZI WATOA AHADI, WASHTUKIWA
HATA hivyo, mapaparazi wetu walimwambia mfanyakazi huyo kwamba kwa muda huo hawana fedha, wangerudi tena jioni na fedha ili kumaliza biashara.
Jibu hilo lilimshtua jamaa huyo na kuwaweka chini ya ulinzi huku akimnyang’anya simu mmoja wa mapaparazi hao.
Aliikagua simu hiyo na kugundua alikuwa akirekodiwa sauti hivyo akafuta sauti hiyo. Pia aliikagua simu hiyo na kubaini meseji za paparazi huyo kumtumia meseji mhariri wake akimwambia upelelezi unakwenda vizuri.
Mfanyakazi huyo alikwenda mbele zaidi kwa kuangalia namba zilizopigwa kwenye simu hiyo na kuona moja ambayo jina la aliyepigiwa lilimaliziwa na paparazi, mfano; Paschal Paparazi, jamaa akashtuka zaidi.
Kama vile haitoshi, jamaa huku presha ikiwa juu, aliingiza mkono kwenye mifuko ya suruali ya mapaparazi wetu na kukutana na vitambulisho vyenye nembo ya Global Publishers & General Enterprises.
“Sikieni, mimi sitaki maneno na nyinyi, nawaomba muondoke eneo hili haraka sana, mmenifanya mimi ni mtoto siyo?” alisema mfanyakazi huyo. OFM iliondoka kwa mafanikio makubwa kwani ilithibitika biashara hiyo ipo.

Posted by Unknown on 1:42 AM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for "Tanzania na Biashara ya Viungo vya Maiti."

Leave a reply

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...